Lwandamina atimuliwa Azam FC

477

Azam FC imefikia maamuzi ya kumfuta kazi ya ukocha klabuni hapo aliyekuwa George Lwandamina na msaidizi wake Bahati Vivier.

Maamuzi ya kumfuta kazi kocha huyo yamefikiwa baada ya matokeo ya sare tasa ya mchezo wa Azam waliokuwa wenyeji dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliopigwa jana katika dimba la Chamazi.

Lwandamina anafutwa kazi ikiwa ni wiki chache tangia kuingia makubaliano ya kuongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kukitumikia kikosi hicho cha Wanarambaramba wa Azam.

“Nimepokea taarifa hiyo lakini naenda kuonana na viongozi wa klabu, ni maisha yetu ya mpira,” amesema Lwandamina.

Azam mpaka sasa wanashika nafasi ya saba wakiwa na pointi 11 baada ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza mechi tatu.

Author: Asifiwe Mbembela