Mashemeji derby: Ujanja wa Ingwe waishia kwa Muguna, Kahata

263

Waliingia uwanjani na ujanja wa kuwanyuka watani wao wa jadi Gor Mahia kisha kutia mfukoni Kshs10,000 marupurupu ya kushinda derby ya Mashemeji lakini AFC Leopards ilikoseshwa ujanja na mabao ya Kenneth Muguna na Francis Kahata wakipoteza 2-0 uwanjani Kasarani alasiri ya leo Jumamosi.

Kocha wa Gor Mahia Otkay ashinda Mashemeji derby yake ya kwanza na Gor

Muguna aliipa Gor uongozi dakika ya 16 baada ya mabeki wa Ingwe kuzembea kuondoa eneo hatari krosi ya Boniface Omondi. Kahata naye aliandikisha jina lake kwa mara ya kwanza kwenye debi dakika ya 76 akitia nyavuni hikabu iliyomwacha kipa wa Ingwe Eric Ndayishimiye akizubaa.

Ushindi huu unawavusha mabingwa hawa watetezi hadi nafasi ya pili kwenye jedwali kwa pointi 22, tatu nyuma ya kiongozi Mathare United japo na mechi moja mkononi.

“Huwa sitizami jedwali jinsi linakaa kwa mechi kumi sasa,” alidokeza kocha wa Gor Hassan Oktay kwenye mahojiano baada ya mechi. “Kwetu ni kukusanya pointi tatu kila mechi na nafurahi na ushindi huu wangu wa kwanza kwenye debi, ni motisha kubwa tukielekea Angola mechi ya kombe la shirikisho Jumatano hii ijayo.”

Kocha wa Leopards hakuwa na majibu uwanjani Kasarani

Kocha mgeni wa Ingwe, Mnyarwanda Andre Casa Mbungo alihamakishwa na kichapo cha pili tangu kuwahi majukumu ya mabingwa hawa mara kumi na tatu wa ligi kuu ya KPL. “Mwezi Machi nina nafasi ya kusajili wachezaji wa kuisaidia timu lakini kwa sasa lazima niwatengeneze hawa waliopo manake ni wazuri,” alikiri.

Ingwe wapo nafasi ya kumi na tano na pointi kumi, moja tu mbele ya Chemelil Sugar, Mount Kenya United na Posta Rangers walio mkiani japo wana mechi wiki ya kesho.

Derby ya leo, ya 90 katika historia ya timu zote mbili ilianza kwa mbwembwe huku kikosi cha Ingwe kikifika uwanjani dakika ishirini kabla ya saa nane na kupitia lango nambari 19 ambapo timu zote zinazochuana hupitia lakini ajabu ni kwamba mahasimu wao walifika saa nane na robo na kutumia lango nambari 18 ambalo kwa kawaida huwa halipitiki siku za mechi.

Mashabiki wa Leopards walishangilia timu yao licha kichapo

Ujanja huu wa Gor uliwashinda Ingwe hadi uwanjani pindi tu mwamuzi wa siku Anthony Ogwayo alipuliza kipenga cha kuashiria ngarambe kuanza. Gor ilishambulia kupitia Muguna na Jacques Tuyisenge dakika za mwanzoni lakini kipa wa Ingwe Ndayishimiye alionekana imara hadi dakika ya 16. Bao la Tuyisenge dakika kumi za mwisho wa mchezo lilikataliwa eti alikuwa ashaotea tayari japo video zinaonyesha alikuwa sahihi.

Author: Vincent Stephen