MO Dewji atoa neno alichofanyiwa Barbara

216

Mwekezaji wa klabu ya Simba Mohammed Dewji maarufu kama MO amesema ni aibu kuona kile kilichotokea Jana Jumamosi Disemba 11,2021 kwenye mechi ya Watani wa Jadi baina ya Simba wenyeji na Yanga ambapo Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo alizuiliwa kuingia kukaa eneo la VVIP.

Kauli ya MO inakuja ikiwa ni siku moja tangia, walinzi wa geti la kuingilia sehemu ambayo wanakaa watu wa VVIP kumzuia Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez kuingia kwa kile ambacho baadaye Shirikisho la Kandanda nchini TFF lilieleza kuwa Mtendaji huyo alikiuka msingi wa makubaliano ya klabu hizo Simba na Yanga) na Bodi ya Ligi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter MO amesema “nimesikitishwa sana na kitendo alichofanyiwa CEO wa Simba cha kuzuiliwa kuingia kwenye eneo la VVIP katika mchezo wa jana”.

MO ameongeza kuwa kwa nafasi ambayo anayo Barbara hakutegemea kama lililotokea lingetokea “Kwa nafasi ya uongozi aliyonayo Ceo ni jambo la aibu kwa soka letu kukutana na kadhia kama ile. Kumvunjia heshma CEO, nikuvunjia heshma taasisi ya Simba”.

Baada ya Barbara kuzuiliwa inaelezwa kuwa aliamua kuondoka uwanjani hapo ingawa kwa taarifa ya TFF inaeleza kuwa Mtendaji huyo aliruhusiwa kuingia pekee yake na siyo familia yake aliyokuwa ameongozana nayo.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Almas Kasongo alisema kuwa utaratibu wa kuingia uwanjani hapo kwenye jukwaani la VVIP lilikuwa la watu maalumu ambao wanahusika klabu hizo na hayo yalikuwa makubaliano baina ya klabu ambapo timu mwenyeji alipewa tiketi 40 wakati Yanga aliyekuwa mgeni katika mchezo huo alipewa tiketi 30.

Author: Asifiwe Mbembela