Simba kitete bila Morrison, Bwalya Kagera

364

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara klabu ya Simba imesafiri na kutua salama mpaka mji wenye sukari yake, Kagera huku kitete kikiwa kinapanda na kushuka baada ya taarifa ya madaktari kusema kuwa uwezekano wa mtukutu Bernand Morrison na kiungo maestro Rally Bwalya kucheza kuwa finyu.

Kitete cha watetezi hao wa TPL kinakuja kufuatia mchango chanya kwenye mechi za mashindano uliopo kichwani na miguuni mwa nyota hao wawili mmoja raia wa Ghana Afrika Magharibi na mwingine Zambia Kusini mwa Afrika (Bwalya).

Simba inategemea kumenyana na Kagera Sugar Jumamosi Disemba 18 bila pia huduma ya mshambuliaji na nahodha wa kikosi hicho John Raphael Bocco.

Mbali na wachezaji hao watatu, mabingwa wa nchi wataendelea kukosa huduma ya Chris Mugalu na Taddeo Lwanga ambao ni majeruhi wa muda mrefu, wengine walioachwa Dar ni; Erasto Nyoni, kipa, Jeremiah Kisubi, Israel Mwenda na Pascal Wawa.

Simba inashika nafasi ya pili katika msimamo na kama itashinda mechi ya kesho itaiengua Yanga kwa muda, kwani itafikisha pointi 21. Yanga inayoongoza msimamo imekusanya pointi 20 kupitia mechi nane kama ilizocheza Simba.

Author: Asifiwe Mbembela