Wiki ya Mwananchi Yanga, Usipime!

543

Yanga imesema imekusudia kuzindua Wiki ya Mwananchi Agosti 22 katika visiwa vya Karafuu Zanzibar ambapo kilele chake kitakuwa Agosti 29 katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ndiyo siku ambayo nyota wote watakuwa hadharani

Akizungumza kuelekea tukio hilo ambalo limekuwa likigusa maisha ya watu wenye mazingira magumu, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa malengo makubwa ni kushirikiana na mashabiki na wapenzi wa timu hiyo katika kutoa misaada maeneo kusudiwa.

“Uzinduzi utafanyika Zanzibar Jumapili hii, hivyo niwaombe mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga,visiwani humo wajiandae kwa tukio hili kubwa ambalo litaambatana na mambo mbalimbali ya kijamii,” amesema.

Aidha Bumbuli amewataka wanachama, mashabiki wa Yanga kukaa tayari kwa ajili ya Wiki ya Mwananchi na kuwahimiza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

“Tunawaomba wajitokeze kushiriki kikamilifu katika Wiki ya Mwananchi , lakini pia wajipange kujumuika nasi hapa Dar es Salaam kwa ajili ya kilele Agosti 29 ambapo watapata fursa ya kuona kikosi chao cha msimu ujao,,” amesema Bumbuli.

Hii ni mara ya pili ufunguzi wa Wiki ya Mwananchi kuanzia visiwani humo ukiambatana na shughuli mbalimbali za kijamii na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Kikosi cha Yanga kwa sasa kiko nchini Morocco kilipoweka kambi kujiandaa na Ligi Kuu Bara na mashindani ya kimataifa.

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu hiyo ni Djigui Diarra, Erick Johora, Djuma Shaban, Jesus Muloko, David Bryson, Dickson Ambundo, Khalid Aucho, Heritier Makambo na Fiston Mayele.

Author: Asifiwe Mbembela