Aguero atundika daluga Barcelona

248

Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Sergio Kun Aguero leo Jumatano (Desemba 15) ametangaza rasmi kustaafu soka kutokana na tatizo la moyo.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 33 amesema, amechukua maamuzi hayo magumu kwa kuheshimu ushauri wa kiafya aliopewa na madaktari wa FC Barceliona ambao wamekua wakimuangalia tangu alipogundulika na tatizo la moyo.

Aguero amesema: “Huu mkutano ni maalumu kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe kwamba nimeamua kusimama kucheza mpira. Ni wakati mgumu na maamuzi ambayo nimeyachukua ni kwa ajili ya afya yangu hii ni sababu kubwa.”

Aguero alianza kupata maumivu katika mchezo dhidi ya Alaves uliomalizika kwa sare ya 1-1 mwezi Oktoba 2021.

Ikumbukwe kwamba Aguero alijiunga na FC Barcelona msimu huu akiwa mchezaji huru kwa dili la miaka miwili akitokea Manchester City ambapo huko aliweka rekodi ya kuwa mzee wa kutupia katika misimu 10 ambayo amecheza.

City ilipata saini ya Aguero 2011 akitokea Klabu ya Atletico Madrid na aliweza kufunga bao la maajabu katika msimu 2011/12 na kuipa timu hiyo taji la kwanza la Ligi Kuu England.

Jumla alipachika mabao 260 katika timu na alicheza jumla ya mechi 390, ni mataji matano ya Ligi Kuu England alitwaa, mataji sita ya League Cup.

Author: Bruce Amani