John Terry atundika daluga

149

Nahodha wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya England John Terry ametangaza kuachana na soka. Terry mwenye miaka 37, aliondoka Aston Villa katika majira yaliyopita ya joto, baada ya kuichezea klabu hiyo kwa msimu mmoja.

Kabla ya hapo, alicheza na klabu ya Chelsea kwa misimu 22, ambako alishinda mataji matano ya ubingwa wa ligi, matano ya kombe la FA, ligi ya mabingwa Ulaya, Champions, ligi ya Europa na matano ya kombe la Ligi, akiwa amecheza zaidi ya  mara 700.

Terry aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram “baada ya miaka 23 kama mchezaji wa soka, nimeamua sasa ni wakati muafaka wa mimi kupumzika”. Aliongeza kuwa, “nilifanya maamuzi mazuri kujiunga na Chelsea nikiwa na miaka 14! Maneno pekee hayatatosha kuelezea umuhimu wa kila mmoja kwenye klabu, na hususan mashabiki. Tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa na nisingeweza kufanikiwa kwa kiasi hicho bila nyinyi”.

Terry pia alicheza mara 78 akiwa na timu ya taifa ya England, na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki miachuano ya kombe la dunia mwaka 2006 na 2010, lakini pia kwenye michuano ya Ulaya mwaka 2004 na 2012

Author: Bruce Amani