Aguero akubali miaka miwili kuitumikia Barcelona

253

Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Sergio Kun Aguero amekubali kujiunga na kikosi cha Barcelona kinachonolewa na kocha Mholanzi Ronald Koeman baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu 2020/21 ndani ya Manchester City.

Mchezaji huyo wa zamani wa Atletico Madrid mwenye umri wa miaka 32, ataondoka katika dimba la Etihad baada ya mchezo wa mwisho wa Manchester City wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya fainali dhidi ya Chelsea Mei 29.

Kwa mjibu wa vyanzo vya ndani vinaelezea kuwa mchezaji huyo aliyekuwa anahusishwa kujiunga na Chelsea, Juventus na PSG amekubali kutua Camp Nou kwa mkataba wa miaka miwili ili kuungana na nyota mwezake wa Argentina staa Lionel Messi.

Hata hivyo, Manchester City wakifanikiwa kumpeleka Aguero Barcelona watakuwa wanapata bonasi za malipo endapo atashinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi chote atakachokuwa klabuni hapo.

Author: Asifiwe Mbembela