Gambia Yafuzu Robo Fainali Afcon 2021, Waitoa Guinea

310

Wakicheza kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON 2021, Gambia wameendelea kuandikisha rekodi baada ya kufuzu kucheza hatua ya robo fainali kwa kuifunga Guinea bao 1-0 mchezo uliopigwa Leo Jumatatu.

Bao pekee la ushindi limefungwa na mshambuliaji wa Bologna inayoshiriki Ligi Kuu nchini Italia Seria A Musa Barrow akimalizia kazi nzuri ya Aly Keita kunako dakika ya 71 ya mchezo.

Pamoja na ushindi huo, Gambia walimaliza mchezo wakiwa pungufu kufuatia Yusupha Njie kuonyeshwa kadi nyekundu dakika tatu kabla ya mbungi hilo kumalizika.

Gambia ambao wanashika nafasi ya 150 kwenye viwango vya Fifa watacheza na mshindi baina ya Comoros au Cameroon katika hatua ya robo fainali ya Afcon 2021 ambapo tayari ubingwa uko rehani baada ya Algeria kutupwa nje hatua ya makundi.

Author: Bruce Amani