Kocha Bandari FC Apongeza Usajili Ulivyofanyika

161

Kocha mkuu wa Bandari FC Anthony Kimani amesema kwa sasa hawasajili mchezaji mwingine na sasa akili yao wanaielekeza kwenye maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu nchini Kenya FKFPL.

Bandari FC ambao walimaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu walipanga wakamilishe kwanza usajili wa ndani kisha ndiyo waanze maandalizi ya msimu ujao.

Majina ambayo yameingia kwenye kikosi hicho ambacho kinakusudia kushindania ubingwa ni James Kinyanjui, Fidel Origa wote kutoka Wazito, Felix Oluoch na Douglas Mokaya wote kutoka Kariobangi Sharks, Enock Momanyi kutokea FC Talanta, Abeid Mudiga kutoka Coast Stima, na Omar Somobwana kutokea AFC Leopards.

“Tumemaliza na maingizo mapya kwenye kikosi chetu. Hata wale ambao wanaondoka pia walitolewa mapema. Kwa kweli nafurahia namna ambavyo tumeendesha usajili wetu”, alisema kocha Kimani.

Mbali na wachezaji ambao wamesajiliwa, Bandari imewaondoa wachezaji sita ambao ni Swaleh Chacha, Hassan Idi, Kevin Kimani, Danson Chetambe, Collins Agade, na Johanna Mwita.

Author: Asifiwe Mbembela