Mashabiki Kuingia Bure Uwanjani Mzunguko

91

Mashabiki wataruhusiwa kuingia bure kwenye eneo lote la mzunguko katika mchezo wa Kundi F kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Taarifa za kuingia bure zimetolewa na Afisa Habari wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo ambaye ameeleza kuwa hali hiyo inatokana wadau mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwanunulia tiketi mashabiki.

Taifa Stars itashuka dimbani katika mchezo utakaoanza saa 2:00 usiku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Uganda Ijumaa Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia nchini Misri, bao pekee la Simon Msuva.

Kwa sasa Taifa Stars inashika nafasi ya pili Kundi F kwa pointi nne, nyuma ya Algeria yenye pointi tisa na mbele ya Niger yenye pointi mbili na Uganda pointi moja baada ya mechi tatu za awali.

Author: Asifiwe Mbembela