Real Madrid yajibu mapigo ya Barcelona, yashinda kwa Mallorca

245

Winga wa Real Madrid Vinicius Junior na beki Sergio Ramos wamehusika kuipandisha Madrid katika nafasi ya kwanza ya msimamo wa ligi kuu nchini Hispania kwenye kandanda ya La Liga baada ya kuichabanga Mallorca 2-0.

Akifunga goli lake la 10 msimu huu, mlinzi wa Kihispania Sergio Ramos alikwamisha mpira nyavuni kwa goli la pili kwa njia ya freekick huku winga wa Kibrazil Vinicius akichopu mpira uliomshinda mlinda mlango wa Mallorca.

Kikosi cha Kocha Zinedine Zidane kinatoshana hivi sasa alama na waliokuwa vinara wa ligi Barcelona kwa pointi 68 ingawa Madrid wanaongozwa kwa sababu wana rekodi nzuri ya timu zilizokutana.

Licha ya kupoteza lakini Mallorca waliandikisha rekodi ya aina yake ya kumtumia mchezaji kinda mwenye miaka 15 Luka Romero na kuwa mchezaji mdogo zaidi kwenye Ligi.

Mshambuliaji wa Wales Gareth Bale alianzishwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Real tangu Februari isipokuwa hata kwenye mtanange huo alishindwa kuonyesha mchango mkubwa.

Real wamebakiwa na mechi saba, ushindi kwenye angalau kila mchezo unaweza kuwapa ubingwa wa kwanza tangu walipofanya hivyo mwaka 2017.

Author: Bruce Amani