Ronaldo afunga penati mbili na kuwapa pointi moja vinara Juventus dhidi ya Atalanta

258

Mshambuliaji wa Juventus Cristiano Ronaldo ameinusuru timu hiyo kukumbwa na kipigo cha aibu kutoka kwa Atalanta baada ya kulazimisha sare ya goli 2-2 ndani ya ligi ya Serie A.

Goli mbili za penati ziliipa Juventus alama moja na kuwafanya kuendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya alama nane dhidi ya timu iliyonafasi ya pili Lazio.

Pengine kilikuwa kiwango kibovu zaidi kwa Juventus kwa msimu huu ambapo walikuwa katika dimba la nyumbani na walishindwa kumiliki mpira kwa dakika nyingi za mchezo huo.

Duvan Zapata na Ruslan Malinovskiy walikuwa nyota wa mchezo kwani kila mmoja alihusika katika goli moja wakifunga kwa tofauti ya vipindi.

Hata hivyo, Ronaldo aliviokoa Kibibi kizee cha Turin kwa kufunga goli mbili na kufikisha goli 28 katika mechi 28 za Ligi Kuu Serie A.

Katika hatua nyingine, timu iliyonafasi ya pili Lazio ilijikuta ikiangukia pua kwa kukubali kichapo cha 2 – 1 kutoka kwa Sassuolo.

Author: Asifiwe Mbembela