Sakata na ‘wakili msomi’ Morrison kati ya Yanga na Simba laanza tena

493

Sakata la winga wa Simba Bernard Morrison ni kama limeanza upya au limeibuliwa tena baada ya Yanga kusema kutocheza kwake kwenye mechi mbili za Wekundu wa Msimbazi ni kwa sababu amewekewa “stop” na Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Soka ya Kimataifa (CAS).

Hiyo ni baada ya Yanga kupeleka mashitaka yao CAS ikiomba sakata hilo kusikilizwa upya baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumuamuru Morrison kuwa mchezaji huru na yeye kuamua kuibukia ndani ya Simba.

Kamati hiyo iliamuru Mghana huyo kuichezea Simba baada ya kubaini mkataba wake wa awali na Yanga kuonekana una mapungufu, maamuzi hayo yaliwafanya viongozi wa Yanga kukimbilia CAS kwenda kukata rufaa.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela imesema kuwa baada ya kupokea barua kutoka CAS sasa wanasubiria kumookea mwamuzi wa kesi hiyo mwezi Januari.

Upande wa klabu ya Simba haujatoa taarifa yoyote endapo wamepokea barua hiyo au la, lakini kukosekana kwa Bernard Morrison kwenye mechi ya Mbeya, dhidi ya Mbeya City na FC Platinum kule Harare Zimbabwe kunaongeza fununu kuwa huenda kuna ukweli juu ya hili.

Author: Asifiwe Mbembela