Yanga hii tema mate! yafuata nyayo za Simba

Kuna usemi husema ukitaka kuruka lazima uagane na nyonga, usemi huu mara nyingi huonyesha namna ambavyo kila unalolihitaji kulifanya ni lazima kuwepo kwa mipango na mikakati inayotekelezeka.

Inawezekana usiagane na nyonga lakini ukafika pale ulipokusudia ingawa hutokea mara chache.

Muda mwingine kuikubali hali halisi ya maisha hasa pale ulipokuwa juu huwa vigumu/ngumu. Yanga walikuwa juu na kufanikiwa kutawala soka la Tanzania. Ikatwaa mataji matatu mfululizo ya VPL. Ikatwaa FA na soka tamu lililopewa jina la “Kampa kampa, Tena chini ya mwandamizi Thaban Sinkara Kamsoko”.

Hali ikabadilika ghafla, upepo ukabadilika, maisha yakabadilika ingawa wao wenyewe Yanga wakakataa kuikubali hali yao kwa wakati huo.

Wakati hayo yakitokea, upande wa pili Simba wakawa vizuri wakatwaa mataji na kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Yanga enzi hizo.

Katika miaka takribani minne Yanga waliyumba hasa, licha ya kuyumba kwao walikuwa hawaikubali hali hiyo, kila mwanzo wa msimu walijitapa kuwa sawa mbali na kupitisha bakuli la changizo.

Hapa ndipo usemi wa kuagana na nyonga unafikia, baada ya kujitekenya na kucheka wenyewe kwani walisema wako vizuri ingawa undani walikuwa wanaujua.

Mwishoni mwa msimu uliopita 2019/20 walikaa chini na kuangalia msingi wa kushindwa kwao na fedha ikaongezeka(kuagana na nyonga) kwa maana waliketi wakasema ili turudi katika zama zetu tufanyaje na kisha sasa wanaruka kwa kishindo.

Kitako chao kikaja na wachezaji wazuri jambo ambalo misimu kadhaa nyuma walikuwa na wachezaji wa kawaida tena wengine wakuokoteza, sasa kushinda ubingwa mbele ya timu iliyofanya usajili mithili ya Simba na Azam ilikuwa inawawia vigumu.

Mzunguko wa kwanza umemalizika bila kupoteza mechi 17, mechi 13 imeshinda 4 sare vipigo 0. Leo sio ajabu tena kumuona mchezaji kama Michael Sarpong, Haruna Niyonzima, Farid Musa, Zawadi Mauya, Carinhos kuwa nje lakini bado ya Yanga wanashinda.

Hii ni kwa sababu ya kuagana na nyonga, awali walikuwa walazimisha kupaa bila kuangalia misingi yake.

Ili uwe bora ni lazima uwe na ubora sawa na mpinzani wako au zaidi, sasa Yanga waweza angalau kufikia anga za Simba yaani kuwa na kikosi kipana chenye “balasi”, fedha kuwepo pamoja na hamasa.

Hivyo ndivyo, Yanga ilivyo kwa sasa, imekubali kuziaga nyonga zao na sasa ukiwaangalia wanaruka vyewa. Hawajatwaa ubingwa lakini kuna maendeleo kulinganisha na misimu minne nyuma.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares