Uganda kucheza na Nigeria mchuano wa kirafiki

173

Shirikisho la Kandanda la Uganda – FUFA limethibitisha kuwa timu ya taifa Uganda Cranes itashuka dimbani dhidi ya Super Eagles wa Nigeria katika uwanja wa Stephen Keshi mjini Asaba Novemba 20 mwaka huu. Mechi hiyo itachezwa siku tatu baada ya mpambano wa kufuzu katika fainali za AFCON 2019 kati ya Uganda na Cape Vere katika uwanja wa Namboole.

“Kikosi cha watu 30 kitaondoka Novemba 18 2018 kuelekea Nigeria, kisha wachezaji wa soka la kulipwa katika nchi za kigeni wataondoka kwenda kujiunga na vilabu vyao” amesema Meneja wa Mawasiliano wa FUFA.

Mataifa hayo mawili yanatarajiwa kuviweka uwanjani vikosi vyao vya kwanza. Uganda na Nigeria zilikutana mara ya mwisho mwaka wa 2015 wakati Uganda ilipoipiku Nigeria 1-0 katika uwanja wa Ibo Akwa katika mchuano mwingine wa kirafiki.

Timu zote zinawania tikiti ya kushiriki katika fainali za AFCON nchini Cameroon hapo mwakani.

Nigeria kwa sasa inaongoza Kundi E na pointi 9 kutokana na mechi zao nne. Mchuano ujao utakuwa dhidi ya Afrika Kusini mjini Johannesburg.

Uganda pia wanaongoza kundi lao la L na pointi 10 kutokana na mechi zai nne za kwanza na watawaalika Cape Verde katika mchuano ujao.

Author: Bruce Amani