Yanga yachabangwa na Coastal Union 2-1, waondoka vichwa chini

295

Kikosi cha Coastal Union kinachoshiriki michuano ya Ligi Kuu Nchini Tanzania kimefanikiwa kuondoka na alama tatu katika mchezo wa VPL dhidi ya Yanga mtanange uliopigwa kwenye dimba la CCM Mkwakwani Mkoani Tanga.

Yanga ambayo ilikuwa haijapoteza mchezo wowote kabla ya mechi ya leo walianza kupoteza nguvu baada ya kukosa tuta lililopigwa na winga Tuisila Kisinda baada ya hapo Eric Msagati akaitanguliza Coastal Union.

Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, Yanga walisawazisha bao hilo kupitia kwa Tuisila Kisinda akirekebisha makosa yake.

Ungwe ya pili ilikuwa na shubiri zaidi kwa yanga baada ya Mudathiri Hamis kufunga bao la ushindi kwa shuti kali likimshinda mlinda mlango Farouk Shikalo

Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union kufikisha alama 26 wakati Yanga wakibakia na pointi 49 katika nafasi ya kwanza.

Author: Asifiwe Mbembela