Waziri Bashungwa atoa agizo TFF kuhusu Waamuzi

350

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kuwachukulia hatua waamuzi wa mpira wanaoonekana kufanya mambo ya hovyo katika kuamua michezo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inayoendelea.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Desemba 05, 2021, wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Mtwara katika kilele cha mashindano ya kitaifa ya Michezo na Sanaa ya vyuo vya ualimu UMISAVUTA yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Novemba 29, 2021.

Waziri Bashungwa amesema licha ya Ligi Kuu ya Tanzania kuendelea vizuri lakini kumekuwepo na waamuzi wanaofanya mambo ya hovyo ambayo siyo tu yanashusha adhi yao lakini yanavunja imani, amani na mioyoo ya wachezaji na mashabiki wa timu zinazofanyiwa mambo hayo.

Kauli ya Waziri Bashungwa inakuja kipindi ambacho kumekuwa na malalamiko mengi ya wadau wa soka nchini juu ya maamuzi ambayo yamekuwa yakitiliwa doa hasa kwa michezo ambayo imekuwa ikitazamwa sana, mchezo wa Namungo Fc dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya 1-1, na Simba dhidi ya Geita Gold ya 2-1.

Author: Bruce Amani