Bora Tukacheze Ligi ya Zanzibar – Mwenyekiti Simba

165

Mwenyekiti wa klabu ya Simba Murtaza Mangungu amesema wao kama Simba wako tayari kwenda hata kucheza Ligi nyingine mbali na Tanzania bara kama wataendelea kulazimishwa kutumia nembo ya mdhamini mweza wa Ligi GSM bila kufuata utaratibu na kanuni.

Mwenyekiti wa Wekundu wa Msimbazi Simba Mangungu ametoa kauli hiyo wakati akiongea kwa njia ya simu na Wasafi FM Radio Leo Ijumaa Disemba 10 ambapo amesema wao wanaamini kuwa wanasimamia sheria na siyo kufuata hisia za mtu.

Amesema kuwa wao kama Simba waligoma kushiriki mkutano na Waandishi wa Habari kwa sababu kulikuwa na nembo ya mdhamini ambaye ni GSM kwenye moja ya mabango kwenye mkutano huo jambo ambalo lilipekea kususia mkutano kabla ya baadaye kocha wa Simba kuzungumzia maandalizi ya mchezo kupitia mitandao ya kijamii ya klabu.

Mangungu ameongeza kwa sababu hawakupewa taarifa mapema ili kujua wao watanufaika vipi na huo udhamini wanajiona kuwa kwenye haki. Pengine kama wataendelea kulazimishwa kuvaa nembo ya mdhamini huyo mweza wa Ligi (GSM) basi wako tayari kwenda hata kucheza Ligi nyingine mbali na Ligi ya Tanzania Bara, tunaweza kwenda hata Zanzibar.

“Kuna Ligi nyingi, si bora tukacheze Ligi ya Zanzibar…”

Mchambuzi wa Kandanda nchini Charles Abel akizungumzia suala hilo, amesema kuwa makosa ambayo yametokea kwa hivi sasa yanatoa mwanga wa kufanyika marekebisho kwenye kanuni za Ligi.

Kauli ya Mangungu inafuatia sintofahamu baina ya Simba na Bodi ya Ligi/TFF juu ya mabango ya GSM ambaye aliingia udhamini na TFF wa takribani bilioni 2 na kuwa mweza wa ligi baada ya benki ya NBC.

Author: Asifiwe Mbembela