Chama, Onyango waikosa Namungo, Kocha asema hakuna tatizo

233

Klabu ya Simba baada ya kufika na kufanya mazoezi salama mkoani Lindi Leo Jumamosi Mei 29 itapepetana vikali na timu mwenyeji Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa dimba la Ruangwa majira ya saa 10 jioni.

Kuelekea mtanange huo, Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema kikosi cha wachezaji 20 waliosafiri na timu wako tayari kwa ajili ya mchezo wa Leo.

Matola ameongeza kuwa wanafahamu mchezo utakuwa mgumu, Namungo ni timu nzuri hasa inapokuwa nyumbani lakini lengo ni kuhakikisha alama tatu zinavunwa.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama hapa Lindi, wachezaji wote wako vizuri. Tunajua haitakuwa mechi rahisi Namungo ni timu nzuri hasa inapocheza nyumbani lakini sisi tumejipanga kuondoka na alama zote,” amesema Matola.

Matola amesema katika mchezo wa kesho tutakosa huduma ya wachezaji Joash Onyango, Clatous Chama na Ibrahim Ame kutokana na sababu tofauti lakini hakuna kitakachoharibika kwani lilikuwa linafahamika mapema.

“Tutakosa huduma ya Onyango ambaye bado afya yake haijaimarika vizuri, Chama ameaga ana matatizo ya kifamilia na Ame anayetumikia adhabu ya kufungiwa,” amesema Matola.

Mchezo wa kwanza kwa Simba dhidi ya Namungo ambapo licha ya mechi kubakia tisa kumalizika kwa VPL bado zilikuwa hazijakutana kutokana na ushiriki wa kimataifa.

Simba ni kinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na alama 61 katika mechi 25 sawa na Yanga Sc kialama tofauti ya michezo iliyocheza 29, wakati Namungo ikiwa nafasi ya 8 na pointi 40.

Author: Asifiwe Mbembela