Kenya yavunja shirikisho la kandanda – FKF kwa madai ya rushwa

134

Kenya leo imelivunja shirikisho la kitaifa la kandanda – FKF kuhusiana na madai ya rushwa na kusema huenda ikawafungulia mashitaka maafisa wanaohusishwa. Hatua hiyo imepingwa haraka na mkuu wa FKF aliyetimuliwa Nick Mwendwa ambaye amekanusha kuwepo na makosa yoyote. Hatua hiyo imepingwa haraka na mkuu wa FKF aliyetimuliwa Nick Mwendwa ambaye amekanusha kuwepo na makosa yoyote.

Waziri wa Michezo Amina Mohamed amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchunguzi wa serikali katika fedha za FKF kufichua kuwa lilishindwa kuthibitisha hesabu za fedha zote lililopokea kutoka kwa serikali na wafadhili wengine. Waziri ametangaza kamati ya muda kuendesha masuala ya shirikisho hilo hadi uchaguzi utakapoandaliwa katika miezi sita.

Lakini Mwendwa ameapa kupambana dhidi ya hatua hiyo. Amesema hawakubali uamuzi wa wizara ya michezo na kuwa yeye bado ni mwenyekiti wa FKF na wataendelea na majukumu yao. Uchunguzi wa serikali ulionzishwa wiki mbili zilizopita ulitaka kujua kama dola milioni 2.2 ilizotoa kwa shirikisho hilo zilitumika kama ilivyonuiwa kuiandaa timu ya taifa Harambee Stars kwa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2019 nchini Misri.

Uamuzi huo wa kuwasimamisha kazi maafisa wa FKF huenda ukaiweka Kenya kwenye msuguano na FIFA ambayo inapiga marufuku serikali kuingilia masuala ya mashirika ya kandanda nchini. Mohamed amesema Kenya iliifahamisha FIFA kuhusu matokeo ya uchunguzi huo.

Author: Bruce Amani