Simba yaduwazwa kwa Mkapa na Jwaneng Galaxy ya Botswana

Mabingwa wa Ligi Kuu nchini Tanzania klabu ya Simba imetolewa rasmi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kukubali kufungwa goli 3-1 na Jwaneng Galaxy FC ya Botswana katika mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi hiyo mtanange uliopigwa Leo Jumapili Octoba 24, dimba la Benjamin Mkapa Jijini DSM.

Simba imetolewa kikanuni (bao la ugenini) kwani mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa katika dimba la Taifa la Botswana wiki moja iliyopita ilishinda bao 2-0 lakini kwenye mechi ya pili mambo yakawa tofauti baada ya kuruhusu goli tatu na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3.

Kipindi cha kwanza cha mechi hiyo, Simba ilitawala vyema na kulishambulia mara kwa mara lango la Jwaneng lakini Ubora wa kipa wao Ezekiel Morake uliifanya Simba kuondoka goli moja lililofungwa na Rally Bwalya dakika ya 40 akimalizia pasi ya Benard Morrison.

Mchezo huo ukabadilika ungwe ya pili baada ya Simba kufanya mabadiliko ya mchezaji mmoja kutoka kwa Hassan Dilunga na kuingia kwa Peter Banda wakati Jwaneng walimtoa Themba Dhladhla na Vicent Sesinyi na nafasi zao kuchukuliwa na Tshephang Boithatelo na Rudath Wendell.

Dakika moja baada Wendell aliisawazishia Jwaneng na kuongeza bao lingine ndani ya dakika nne pekee huku yote yakitokana na uzembe wa walinzi wa pembeni na katikati.

Bao ambalo limewapelaka Jwaneng Galaxy hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika limefungwa na Gape Mohutsiwa akimalizia mpira wa krosi wakati muda wa jioni ukiwasili mkononi mwa mwamuzi.

Mpaka dakika 90, wenyeji Simba bao 1-3 Jwaneng Galaxy.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends