Stars Kushuka Dimbani Kuivaa Uganda Kufuzu AFCON

129

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani Leo Jumanne kucheza na timu ya taifa ya Uganda, The Cranes katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Bingwa Afrika AFCON ukiwa ni mchezo wa nne hatua ya makundi.

Mchezo huo utakaoanza saa mbili usiku, mashabiki wameruhusiwa kuingia bure uwanjani baada ya kununuliwa tiketi na wadau wa soka kwenye eneo lote la mzunguko mbali na VIP zote ambazo kutakuwa na gharama.

Stars ili kujiweka kwenye mazingira ya kufuzu italazimika kushinda wakati Uganda wenye alama moja katika kundi ili kufufua matumaini ya kwenda Ivory Coast lazima washinde.

Kuelekea mchezo huo, Ofisa Habari wa TFF Clifford Ndimbo ametoa tahadhari kwa mashabiki kufika uwanjani kushangilia bila kuleta fujo mbalimbali kwa ulinzi utaimarishwa.

Kocha Milutin Sredojević “Micho” wa Uganda akizungumzia mchezo wa leo amesema itakuwa mechi ngumu ambayo inasababishwa na watanzania kuwa na wachezaji wazuri ambao wanacheza mpira wa kulipwa.

Hemed Morocco, kocha msaidizi wa Stars amesema wamewaandaa wachezaji kucheza kwenye presha kubwa ya mashabiki ili waweze kucheza sawa na mipango waliyonayo.

Author: Asifiwe Mbembela