Alcacer airejesha Dortmund kileleni, Bayern yajikwaa

Paco Alcacer alifunga mabao mawili katika dakika tano za mwisho wakati Borussia Dortmund ikiizaba Wolfsburg 2-0 na kukamata tena usukani wa ligi mbele ya Bayern Munich.

Huku ikisalia mechi saba, ni pointi mbili zinazotenganisha timu hizo ambazo zitavaana wiki ijayo uwanjani Allianz Arena.

Alcacer alifunga bao la freekick katika dakika ya 90, kabla ya kusukuma wavuni mpira uliopigwa na Jadon Sancho katika dakika nne za muda wa majeruhi.

Bayern waliangusha pointi ugenini dhidi ya Freiburg, ambapo walitoka nyuma bao moja sifuri na kutoka sare 1-1.

Lucas Holer aliiweka timu ya nyumbani kifua mbele dakika tatu baada ya mechi kuanza kabla ya mshambuliaji wa Poland Robert Lewandowski kusawazisha katika dakika ya 22.

“inakasirisha sana kwa sababu tulikuwa tumefanya vyema kuwafikia Dortmund na sasa tunapaswa kuanza tena,” alisema kocha wa Bayern Niko Kovac.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends