Bayern Munich yapeta kileleni yaichapa Union Berlin na kurejesha mwanya wa pointi nne

228

Kinara wa Bundesliga Bayern Munich amepata alama tatu kiurahisi kwa Union Berlin baada ya kuipiga goli 2-0 katika mchezo mwingine uliokuwa na mwendelezo wa utamaduni mpya wa uchezaji katika ungwe hii ya janga la virusi vya Corona.

Kwenye mchezo uliochezwa bila mashabiki, asilimia kubwa ya watu wakiwa wamevalia barakoa hata namna ya ushangiliaji wa goli ukiwa tofauti, haikuwazuia Bayern Munich kutoka na ushindi huku Robert Lewandowski akiwa mfungaji wa goli la kwanza kwa penati, katika dakika ya 40.

Mlinzi Benjamin Pavard akapigilia msumari wa mwisho kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na mlinzi mweza Joshua Kimmich na kufanya matokeo mpaka tamati, goli 2 kwa Bayern na 0 kwa Union Berlin.

Ushindi huo unafanya Bayern kuwa kileleni kwa tofauti ya alama nne dhidi ya timu inayokamata nafasi ya pili Borrusia Dortmund.

Nyasi na Mipira yote ilikuwa inapuliziwa dawa kuua vijidudu, waokota mipira walikuwa hawakutani moja kwa moja na wachezaji bali walikuwa wanaacha mipira chini yote ni katika kukabiliana na Covid-19.

“Tuna furaha kubwa kwa kuweza kuutawala mchezo vyema na kufanikiwa kuondoka na pointi zote tatu”, alisema mlinda mlango na Nahodha wa kikosi cha Bavarian Manuel Neuer.

“Kucheza bila mashabiki hufanya dakika kuonekana nyingi, mechi huchosha”.

Hata hivyo Pavard baada ya kufunga goli hakuweza kujizuia kushangilia kwani alienda kumkumbatia mchezaji mwezake David Alaba jambo ambalo ni kinyume na Sheria mpya za Bundesliga.

Author: Bruce Amani