Vinara wa Bundesliga Bayern wafungwa na Mochengladbach

185

Vinara wa Bundesliga Bayern Munich wameduwazwa nyumbani na Borussia Monchengladbach katika mechi yao ya kwanza baada ya mapumziko ya baridi
Bayern walikitaja kikosi cha kuungaunga cha wachezaji 11 kwa sababu ilikuwa na wachezaji karibu 12 waliokuwa nje wakiwemo 9 kutokana na maambukizi ya Covid-19.
Robert Lewandowski aliwaweka kifua mbele na shuti kali ikiwa ni bao lake la 20 la Bundesliga msimu huu katikati ya kipindi cha kwanza.
Gladbach ambao wako katikati ya msimamo wa ligi walifunga mara mbili katika dakika nne na kuchukua ushindi
Florian Neuhaus alivurumisha kombora la kusawazisha kwa upande wa wageni kabla ya Stefan Lainer kuwapa ushindi kwa bao la kichwa kutoka mkwaju wa kona.
Hakukuwa na mashabiki katika dimba la Allianz Arena kwa sababu ya vizuzi vya Covid nchini Ujerumani. Licha ya kutawala mchezo mwanzoni, Bayern walipata changamoto bila ya wachezaji muhimu wakiwemo Manuel Neuer, Lucas Hernandez, Leon Goretzka, Leroy Sane, Alphonso Davies na Kingsley Coman. Bayern wako kileleni na pengo la pointi tisa dhidi ya nambari mbili Borussia Dortmund. Gladbach wamesonga hadi nafasi ya 11.

Author: Bruce Amani