Wanaokaa Benchi Wavumilie – Kocha wa Man United Rangnick

126

Kocha wa Manchester United Ralf Rangnick amesema wachezaji wa timu hiyo wanatakiwa kuelewa mazingira ya ufinyu wa nafasi kwenye kikosi hicho licha ya kila mmoja kuwa na mchango kwenye timu hiyo na kuhitaji kucheza mechi baada ya mechi.

Kocha Rangnick amesema hayo baada ya kuibuka kwa uvumi kuwa wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza klabuni hapo hawana furaha na wanahitaji kuondoka.

Miongoni mwa wachezaji ambao wameonekana kutokuwa na furaha wazi wazi ni mshambuliaji wa Ufaransa Anthony Martial ambaye ameomba kuondoka na mazungumzo na Sevilla yanaendelea.

Wachezaji wengine ni Jesse Lingard, Donny van de Beek, Dean Henderson, Eric Bailly na Juan Mata huku mikataba ya Paul Pogba, Mata na Cavani inaelekea mwishoni mwa msimu huu.

Kocha huyo amesema kutokana na idadi kuwa ya wachezaji alionao kwenye kikosi hana namna bali wachezaji ndiyo wanaotakiwa kuelewa hali halisi.

“Tuna idadi kubwa ya wachezaji, kama una namba kama hiyo na wachezaji 11 pekee wanatakiwa kuanza na wengine 3 kuingia kutokea bechi, idadi kubwa inabaki nje au kutotumika kabisa. Lakini hiyo ni hali halisi na inatakiwa kuzoeleka ili upamane”.

Mrithi huyo wa Ole Gunnar Solskjaer Man United mwenye umri wa miaka 63, alipoteza mchezo wake wa kwanza wa EPL mbele ya Wolves wiki iliyopita ambapo imeelezwa kuwa ndani ya kambi ya timu hiyo hali haijatengamaa.

Author: Bruce Amani