Kocha Man United amkana Paul Pogba

373

Kocha wa muda wa Manchester United Ralf Rangnick amesema hatajaribu kumshawishi kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Paul Pogba kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kukitumikia kikosi cha Mashetani Wekundu.

Rangnick amesema kama mchezaji huyo raia wa Ufaransa atakuwa amefanya maamuzi ya kuondoka hatakaa naye kitako kujaribu kumuomba kusalia Old Trafford.

Pogba, 28, ambaye alijiunga na Manchester United kwa mara pili mwaka 2016 kwa dau la rekodi kipindi hicho, la pauni milioni 89 amekuwa akihusishwa kuondoka klabuni hapo na kujiunga na Paris St-Germain au Real Madrid baada ya kandarasi yake kumalizika Juni 2022.

“Simaanisha kuwa si mchezaji muhimu kuwa naye kwenye timu, la hasha! namanisha kuwa mchezaji anatakiwa yeye mwenyewe apende kubakia”, alisema Rangnick akisema hayo wakati anazungumzia mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Norwich City utakaopigwa Leo Jumamosi Disemba 11.

“Kama mchezaji hashawishiki kuchezea klabu kama Manchester United kwa muda mrefu, sifikirii kama itakuwa inaleta maana kumshawishi mchezaji wa kaliba hiyo”.

Pogba, mshindi wa Kombe la Dunia Urusi 2018, kwa sasa ni majeruhi ambapo amekosa mechi saba za United, hata hivyo kiwango chake kwa Waalimu wawili waliopita Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer wote mara kadhaa walionekana kushindwa kumtumia kutokana na kupanda na kushuka kwa kiwango.

Pamoja na hayo, hajafanya mazoezi na timu baada ya kuja Mwalimu Ralf Rangnick.

Author: Asifiwe Mbembela