Msuva, Samatta waikosa tena Malawi, Kim Poulsen aumiza kichwa

Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars inaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya taifa la Malawi utakaopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni siku ya Jumapili Juni 13.

Ambapo licha ya maandalizi hayo kuingia wiki ya pili bado kuna nyota ambao hawajaungana na timu hiyo kutokana na sababu mbalimbali za kiafya na matatizo binafsi.
Nyota hao ni pamoja na David Bryson wa Azam FC ambaye anasumbuliwa na majeruhi na nafasi yake imechukuliwa na nyota Yohana Nkomola, mwingine ni Simon Msuva ambaye yupo Morocco na kikosi cha cha Wydad Casablanca kikijiandaa na mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pia nahodha Mbwana Samatta bado hajaripoti kambini kwa muda wote ambao kikosi kimeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo huo chini ya Kocha Mkuu, Kim Poulsen.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya kambi ya Stars, hatma ya nyota hao ipo mikononi mwa Kocha Mkuu, Poulsen ambaye bado anaendelea kuumiza kichwa kupata mbadala wao mapema kabla ya mtanange huo.

Baadhi ya wachezaji ambao tayari wameripoti kambini na wameanza mazoezi ni pamoja na Dickson Job, Abdul Suleiman, Dickson Kibabage, Feisal Salum, Juma Kaseja, Mzamiru Yassin, John Bocco, na Edward Manyama.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares