Man United yarejea uwanjani kuiwinda Brighton EPL

135

Wachezaji wa Manchester United wanategemea kurejea katika dimba la Carrington kwa ajili ya kuanza mazoezi Leo Jumatano Disemba 15 baada ya kukosa tizi la Jumapili kulikochagizwa na Covid-19.

United walishindwa kufanya mazoezi Jumapili na Jumatatu yaliyokuwa ni maandalizi ya mchezo wa Jumanne dhidi ya Brentford kabla ya mtanange huo kuota mbawa kutokana na kuibuka kwa kesi nyingi chanya za vipimo vya Covid-19 kwa wachezaji na maofisa.

Kikosi cha kocha Ralf Rangnick kimefanyiwa vipimo asubuhi ya leo na wachezaji wote waliokutwa salama wameendelea na mazoezi.

Licha ya kuanza mazoezi, Mashetani Wekundu watasubiri mpaka siku ya Jumapili kucheza mechi dhidi ya Brighton katika dimba la Old Trafford.

Kutokana na kuibuka kwa kirusi kipya cha Covid-19, Shirikisho la Kandanda England limeviagiza vilabu kurejea katika misingi ya awali ya kujikinga na virusi vya Corona ikiwemo kuvaa barakoa na kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja kwenda mwingine.

Author: Asifiwe Mbembela