Matip, Alisson waongeza mzuka Liverpool kuivaa United.

81

Mlinzi wa kati wa Liverpool Joel Matip na mlinda mlango wa Kibrazil Alisson Becker wamerejea kwenye mazoezi ya pamoja na kikosi cha Liverpool kuelekea mtanange wa watani wa jadi dhidi ya Manchester United utakaopigwa dimba la Old Trafford Octoba 20.

Matip alianza msimu wa 2019/20 katika kiwango cha juu kama alivyomaliza msimu uliopita, alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya nyama za paja huku akikosa michezo miwili ule wa Leicester City(EPL) na Red Bull Salzburg(Uefa).

Upande wa Alisson Becker alikumbwa na kadhia ya majeruhi kwenye mtanange wa kwanza dhidi ya Norwich City Ligi Kuu ya England, majeraha hayo yalimfanya mpaka sasa ameshindwa kuichezea Liverpool na Brazil hata mchezo mmoja.

Wawili hao kurejea kwao kunaonekana kuimarisha kikosi cha Liverpool hata ukiwatazama pale Melwood walionekana kuwa na nguvu mpya.

Mtanange dhidi ya United utakuwa muhimu kwa Majogoo wa Jiji la Liverpool zaidi ambapo watahitaji kufikisha alama 8 tofauti na wapinzani wao Manchester City waliopo nafasi ya pili.

Kikosi hicho ya Jurgen Klopp kimeshinda mechi zote nane za awali huku kikionekana kutamani kuyafikia mafanikio waliyoyakosa kwa muda mrefu ya kutwaa taji la ubingwa wa EPL.

Hata hivyo swali kubwa ni endapo Klopp ataamua kwenda na Becker na kumuacha Adrian ambaye ameonyesha kandanda safi tangu atue klabuni hapo kuokoa jahazi la Liverpool.

David De Gea, Paul Pogba, Wan Bissaka hati hati kuukosa mchezo wa Jumapili kwa Manchester United licha ya Luke Shaw na Anthony Martial kuanza mazoezi na timu.

Author: Bruce Amani