Aston Villa yaitwanga Liverpool 7-2 ikiwa ni kipigo cha historia

540

Historia imeandikwa kwa timu ambayo ilikuwa imekaribia kabisa kushuka daraja msimu uliopita wa 2019/20 kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England Liverpool 7-2 katika mchezo ambao ulikuwa wa namna yake.

Kijana Ollie Watkins wa Aston Villa ameihukumu Liverpool kwa kutupia nyavuni bao tatu (hat-trick) katika ungwe ya kwanza huku nahodha wa kikosi hicho Jack Grealish akitupia bao mbili mbele ya Liverpool katika mtanange wa EPL uliopigwa leo Jumapili dimba la Villa Pack.

Watkins mshambuliaji wa zamani wa Brentford alikuwa hajafunga bao lolote la Ligi msimu huu kabla ya kuandika bao tatu kwenye mechi ya leo ambayo makosa binafsi eneo la ulinzi yameigharimu Liverpool.

Jack Grealish baada ya kutupia mbili kwenye mechi hiyo alikuwa pia ametoa msaada wa bao mbili akiwa miongoni mwa wachezaji bora wa mchezo huo.

Inakuwa mara ya kwanza kwa kikosi cha Liverpool kufungwa bao 7 tangu mwaka 1963 ilipopokea kichapo kizito kama hicho na kinakuwa kipigo cha nne pekee tangu Januari 2019.

Shukrani kwa bao mbili za Mmsiri Mohammed Salah aliyetupia bao hizo za kufutia machozi kufuatia kipigo kwa mabingwa wa Kombe la Dunia ngazi ya vilabu Liverpool..

Mbali na rekodi ya ushindi, bao tatu za Watkins mbele ya Liverpool zinamfanya kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Dimitar Berbatov ya kufunga hat-trick dhidi ya Liverpool, rekodi hiyo imedumu kwa muongo mmoja.

Mbali na kipigo cha Liverpool wikiendi hii pia imeshuhudiwa kipigo kingine cha aibu ambacho vijana wa Ole Gunnar Solskjaer Manchester United wamekutana nacho kutoka kwa Tottenham cha goli 6-1 lakini hiki ni cha aina yake.

Author: Asifiwe Mbembela