Nguli wa riadha Mkenya Ben Jipcho afariki dunia

381

Ulimwengu wa riadha unaomboleza kifo cha mshindi wa medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki ya 1972 mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Ben Jipcho. Jipcho amefariki mapema Ijumaa katika hospitali ya Fountain mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu ambako alilazwa siku tatu zilizopita.

Binti yake Ruth Jipcho amesema mwanariadha huyo lejendari alifariki mwendo wa saa tisa alfajiri katika hospitali hiyo ambako alikuwa katika Chumba cha wagonjwa Mahututi.

Amesema daktari aliyemhudumia alisema hali ya Jipcho ilizidi kuwa mbaya kutokana na viungo kadhaa kushindwa kufanya kazi.

Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki nchini Kenya – NOC-K, Paul Tergat, ameomboleza kifo cha Jipcho akisema ni muanzilishi wa riadha nchini Kenya aliyefungua milango ya ulimwengu kwa wanariadha wa Kenya.

Jipcho alishinda fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Edinburg kabla ya kubeba fedha katika Michezo ya Olimpiki ya Munich 1972 katika mbio hizo hizo.

Mwaka wa 1973, alishinda dhahabu katika mita 5,000 na 3,000 kuruka viunzi na maji katika All Africa Games mjini Lagos, Nigeria.

1974, alibeba dhahabu katika mita 5,000 na 3,000 kuruka viunzi na maji na shaba katika mbio za mita 1,500 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Christchurch, New Zealand.

Author: Bruce Amani