Kante kukaa nje miezi mitatu

88

Kiungo mkabaji wa Chelsea N’Golo Kante atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu akiuguza majeraha aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Manchester United ulioisha kwa United kuibuka kidedea kwa goli 2-0 amesema Frank Lampard.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia na Ufaransa nchini Urusi kukosekana kwake ni pigo kwa The Blues ambao bado wanashiriki mashindano tofauti tofauti hivi sasa Uefa, Kombe la Ligi, na EPL.

“Ana maumivu ya misuli, sawa na yale aliyoyapata tulipocheza dhidi ya Arsenal,” alisema Lampard.

Kikosi cha Lampard kitakuwa na mapungufu katika machaguo ya kuanza hasa katika kipindi hiki cha michuano ya Uefa ambapo itakutana na Bayern Munich hatua ya 16 mkondo wa kwanza Jumanne ijayo kabla ya kurudiana mwezi Marchi 10.

Chelsea, inakamata nafasi ya nne EPL ambapo leo Jumamosi wanakutana na Tottenham ambao wapo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Kante, ambaye ni mshindi wa EPL mwaka 2016 na Leicester City na Chelsea 2017 msimu huu amekubwa na majeruhi ya mara kwa mara akiwa amecheza mechi 16 kati ya 26.

Author: Bruce Amani