Maoni: Ni Liverpool, Man City au Tottenham ubingwa wa EPL?

317

Mbio za ubingwa wa EPL hivi sasa ziko wazi. Liverpool baada ya kutoka sare na West Ham wamefanya Ligi kuu England kunoga na kufikia matamu zaidi. Sio timu mbili tena bali tatu mpaka nne kimahesabu zinaweza kuwa bingwa endapo karata zitachangwa vyema. Manchester City, Liverpool, Tottenham Hotspurs na Chelsea ni timu mojawapo ya zinazoweza kunyanyua kwapa msimu huu 2018/2019.

Wakati huu michezo ikiwa imesalia 13 ambapo Chelsea itahitaji ishinde michezo yake yote kufikisha alama 89 nakuombea timu nyingine shindani kupoteza ili kuweza kutwaa taji hili.

Sasa ukitazama mtiririko wa michezo ya mwezi Januari na siku za mwanzo za Februari utagundua kuna nafasi sawa ya kutwaa ubingwa kulingana na matokeo yanayopatikana hivi sasa. Manchester City ilipoteza mbele ya Newcastle United 2-1, Chelsea ikafa mbele ya AFC Bournemouth na Liverpool akakabwa shati na Wagonga Nyundo wa London West Ham United, hayo ni matokeo yanaoashiria kwenye mechi 13 tunaweza kushuhudia mengi.

Hapa tunaziangalia timu tano zinazopewa kipaumbele cha nani ataibuka mshindi wa marathon hiyo.

Liverpool

Klopp anajaribu kuwapa Liverpool ubingwa wa Ligi katika msimu wake wa tatu

Liverpool ina kamata nafasi ya kwanza ya msimamo ikiwa na alama 62 kwenye michezo 15. Mbali na Manchester City hii ni timu inayopewa zaidi kipaumbele cha kunyakua taji msimu huu baada ya kulikosa kwa zaidi ya maka 27. Imani hii inawajia wengi kutokana na ubora wa Jurgen Klopp pamoja na jicho pevu katika usajili. Tazama Virgil Van Dijk, Allison Becker.  Ushujaa wa Klopp upo mpaka kwenye mfumo ambao umekuwa ukitoa matunda chanya wa 4-3-3 pamoja na 4-2-3-1 kama anajilinda.

Saa hizi kila timu Ulaya inawaza kukutana na Liverpool iliyokamilika, takwimu haziogopi. Changamoto kubwa ambayo haionekana lakini inayoweza kukwamisha ndoto za mashabiki wengi wa Liverpool ni mkosi wa Steven Gerrard na Bredan Rodgers mwaka 2014 ambapo walinusa ubingwa wakashindwa kuutafuna. Hii inaweza isiaminike moja kwa moja lakini wachezaji wa sasa wakirejea matukio ya nyuma na kutazama mkanda wa namna ile wanajikuta na hofu ambayo itapelekea kufanya makosa mengi.

Sababu ya pili ambayo pia Mshambuliaji wa zamani wa Everton ambaye pia ni mchambuzi wa soka Kelvin Joseph Campbell amehofia kuhusiana na Liverpool kutwaa ubingwa huo ni uhaba wa kikosi kipana kwa maana usawa wa viwango kwa wachezaji. Anapoumia Van Dijk nani anaingia? Anapoumia Mohamed Salah au Allison Becker nani atachukua mikoba yake na kuonyesha ubora kama ule?. Mwezi wa pili kuelekea wa tatu sio rafiki kwa wachezaji wengi hivyo inaweza pelekea wakashuhudia ubingwa ukielekea kwingine.

Ukosefu wa wachezaji wenye uzoefu. Hivi sasa Soka la kısasa halihitaji sana uzoefu wala historia ingawa nafasi yake haikwepeki. Katika kikosi cha Liverpool James Milner pekee ana uzoefu katika suala la kucheza ukimtazama mwezako kafanya nini kama ligi ya msimu huu ilipofikika. Wachezaji wengine hawajawai kubeba ndoo ya EPL mbali na kuwa washiriki, hivyo kukosa sauti yenye historia na uzoefu.

Manchester City

Mabingwa Manchester City wanalenga kuhifadhi ubingwa

Kwa upande wa Manchester City ambayo imejikusanyia alama 59 imekuwa na changamoto nyingi.. moja, mifumo yote ya timu hiyo imejengwa nyuma ya Mbrazil Fernandinho. Fernandinho amekuwa mhimili wa City, hata akikosekana kwenye mechi, pengo huonekana. Mara kadhaa Pep Guardiola amekuwa akikiri hili. Uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja, uwezo wa kuhamisha timu. Mwezi huu timu inaingia hatua ya 16 bora anaweza kupata majereha au uchovu utakaopelekea hata mwendo wa kikosi cha “The Citizen” kudumaa hivyo kutoa mwanga kwa Liverpool au Tottenham Hotspurs.

Kuzoelekea kwa mifumo ya Pep Guardiola. Katika msimu wa 2017/2018 ilikuwa nadra sana Guardiola kuhangaika kupata matokeo kwa timu kama Wolvehmpton Wanders au Newscastle United.  Msimu uliopita ilivunja rekodi kwa kufikisha alama 100 lakini msimu huu hata akishinda michezo yote alama mia moja hazitafika. 4-1-4-1, 4-1–2-3 imekuwa mifumo rafiki kwa wachezaji wa City ingawa sasa imeanza kuzoelekea, inaweza ikawa shida katika mbizo za ubingwa.

Katika suala la uzoefu City ina wachezaji ambao wanajua umuhimu na riadha ya ubingwa. Tazama David Silva, Vincent Kampany, Fernandinho na Sergio Kun Aguero ni ngao kwa timu hii.

Hotspurs

Spurs wanakabiliwa na changamoto ya wachezaji kuumia, akiwemo Harry Kane

Tottenham Hotspurs imekuwa ni timu yenye kikosi kidogo kwa maana uwezo wa mchezaji mmoja kutofautiana na mwingine. Harry Kane, Son na Dele Alli hawakuwa sehemu ya kikosi timu ilitikisa na kushindwa kupata matokeo rafiki hivyo kuwa kikwanzo kuelekea marathon ya mwisho katika mechi 13 zilizosalia.

Mauricio Pochetttino amekuwa kocha bora kila mmoja anakiri ingawa linapokuja suala la ubingwa unashindwa kumdhamini, juzi ameshindwa FA anatoa sababu ambayo wachambuzi wameikosoa kutokana na ugumu wa kubeba UEFA au EPL lakini wamewai kutafuna wakashindwa kumeza hivyo bundi anaweza akaendelea kuwatafuna.

Chelsea

Chelsea wanamtegemea Higuain kupachika mabao

Chelsea imekuwa na homa ya msimu, inapanda inashuka ingawa usajili wa Gonzalo Higuian umewaongezea kitu katika timu hiyo. Ina wachezaji wenye uzoefu na ligi mbali na kocha kuwa mpya lakini Eden Hazard, Luiz, Kante ni miongoni mwa wachezaji walioonja radha ya ubingwa.

Alama ilizonazo Chelsea inahitaji zaidi neema na bahati kwani ushindi tu ndio utakaokuwa unatoa matumaini ya ubingwa kwao, hivyo sio rahisi kubeba taji hili msimu huu.

Pamoja na changamoto na faida ya hizi timu hasa kwa alama walizonazo kuelekea ubingwa bado michezo iliyosalia itatoa picha tofauti, lakini pia kuna mechi zinazowahusisha mabingwa watarajiwa atakayeshinda atajiweka mazingira rafiki zaidi.

Mbali na kuhusisha mechi za kukutana wao kwao bado kuna mechi ngumu kwa mfano Manchester City, na Liverpool hazijaenda Old Trafford, Emirates au Wembley.

Je, ni timu gani kuibuka shujaa katika mbio hizi? Mda utahukumu vyema.

Author: Bruce Amani