Maoni: Sakata la GSM Litoe Tongotongo za Bodi Huru ya Ligi

367

Siku chache zilizopita kumekuwa na mijadala mingi juu ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC) Ghalib Said Mohamed ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya GSM kujitoa kwenye udhamini.

Kupitia barua yake kampuni ya GSM imetanabaisha baadhi ya vipengele ambavyo TFF na Bodi ya Ligi imekiuka kutekeleza makubaliano hayo ikiwemo klabu ya Simba kukataa kuweka nembo ya mdhamini mwenza kwenye bega la kushoto pamoja na kutowekwa kwa mabango ya mdhamini mwenza kwenye michezo yote ambayo Simba ilikua mwenyeji.

Awali klabu ya Simba ilihoji juu ya uhalali wa mkataba huo na kuzua gumzo baada ya kugoma kutekeleza vipengele vya mkataba huo mpaka utakapo wekwa wazi.

Danieli Mlimuka Mchambuzi wa Michezo Nchini Tanzania anasema “Sakata la GSM kujitoa kama mdhamini mwenza kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, ni sakata ambalo lina maswali mengi sana ambayo mpaka hivi sasa majibu hayajapatikana na miongoni mwa maswali ni kwamba inawezekanaje eeh klabu tuseme 15 za kwenye Ligi zikawa zimetangaza nembo ya GSM bila kulipwa Shirikisho liliruhusu vipi kitu hiki huku ukizingatia kulikua na mkataba umesainiwa kwa nini mdhamini atangaze kwa miezi mitatu apate exposure..apate mawanda mapana kuonekana kwa kiasi hicho kwa mamilioni ya wantanzania bure na sasa hivi tusikie amejitoa”

Hata hivyo uwekezaji huu ulioneka kuwa na tija kwenye soka la Tanzania kwa kuzingatia timu nyingi za daraja la kati zinakabiliwa na ukata na kushindwa kupata baadhi ya huduma muhimu ikiwemo gharama za usafiri, mishahara kwa wachezaji pamoja na fedha za malazi na chakula.

Licha ya athari hizo, mchakato wenyewe wa kumpata mdhamini mwenza umekuwa ukilalamikiwa. Je, hii inaweza kuwa moja ya sehemu ya mjadala wa kuwa na Bodi Huru ya Ligi?

Ngoja turudi nyuma kidogo, ilikuwa Octoba 9, 2014 Rahim Zamunda Mmiliki wa timu ya Afrikan Lyon aliwahi kusema “Bodi ilikuwa na kanuni zake, na kanuni za Ligi ambazo klabu zilikubaliana ni kwamba, kila msimu unapokuwa umemalizika, klabu sita za juu ‘ Top Six’ ndizo zitaingia moja kwa moja katika Bodi ya ligi”.

“Mwenyekiti au makamu wake timu yake itakuwa nje ya nafasi sita za juu atakuwa amepoteza nafasi yake katika Bodi ya Ligi. Vile vile kabla ya msimu mpya kuanza, klabu zinatakiwa kukutana katika mkutano mkuu ambao utajadili namna Ligi ilivyomalizika na faida au hasara zilizopatikana, lakini Ligi imekwisha na hilo halijafanyika, timu hazijakutana kujadili mambo muhimu yaliyotokea msimu uliopita”- Zamunda, Mmiliki wa Afrikan Lyon.

Kiongozi huyo wa Lyon alizungumza kwa kina kuhusu sakata la maagizo ya TFF kudai makato ya 5% kutoka kwa wadhamini kwa klabu za Ligi Kuu huku akitoa ufafanuzi ni namna gani Bodi ya ligi isivyo huru. Hapa tunajifunza kuwa ili tuwe na Ligi imara lazima pia tuwe na bodi imara ya ligi.

Disemba 8 wakati seke seke la klabu ya simba kugoma kutekeleza mkataba wa GSM na TFF Mchambuzi wa michezo Oscar Oscar kupitia kipindi cha Sport HQ alisema “Bodi ya Ligi ni kama kamati ya harusi tu wanatoaje ufafanuzi wa mkataba ambao wao hawakusaini Bodi ya Ligi ni kama Simba tu hawafahamu chochote.”

“Bodi ya Ligi inapaswa kuwa huru sio kuwa chini ya mamlaka ya TFF.” -Oscar Oscar Mchambuzi wa Mpira.

Kwa mfumo wa sasa Bodi ya Ligi ni kama kinda la ndege ambalo husubiria kulishwa kila kitu na mama yake.

TFF imekuwa na Mamlaka makubwa kiasi ambacho Bodi haiwezi kufanya jambo lolote bali kwa maelekezo ya TFF. Bodi imekuwa kivuli. Pengine kutokea kwa matatizo kama haya ya GSM kujitoa linaweza kutukumbusha umuhimu wa kuwa na Bodi huru ambayo ndiyo itakuwa karibu na klabu lakini Shirikisho la Kandanda nchini TFF linaweza kubakia kuwa wasimamizi wa shughuli zote.

Mara kadhaa mifano ya Mataifa ya Ulaya mathalani England imekuwa ikitumika kuonyesha namna ambavyo Bodi ya Ligi inafanya kazi kwa kusimamia vijishughuli vyao kama klabu kwa sababu hata mfumo wa uongozi pia unaangukia huko.

Kuwa na Bodi huru si kwamba itamaliza mapungufu yote ya soka letu bali kwa kiasi tu, kwa sababu kumekuwa na makosa mengine ambayo yanalazimishwa na weredi na kufuata sheria.

Ukiruhusu kutumia busara sehemu ambayo sheria iko wazi, utazidi kupiga hatua mbili mbele, tatu nyuma.

Author: Asifiwe Mbembela